Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Sherehe za kuapishwa kwa Rais Dkt. Mwinyi zimefanyika leo, tarehe 01 Novemba 2025, katika Uwanja wa New Amaan Complex, Mkoa wa Mjini Magharibi, ambapo Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mheshimiwa Jaji Khamis Ramadhan Abdallah, alimuapisha Rais Dkt. Mwinyi.
Dkt. Mwinyi ameapishwa kufuatia ushindi mkubwa alioupata katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika tarehe 29 Oktoba 2025, ambapo alipata kura 448,892 sawa na asilimia 74.8 ya kura zote halali.
Mara baada ya kuwasili uwanjani, Rais Dkt. Mwinyi alipokelewa kwa shangwe na nderemo kutoka kwa maelfu ya wananchi waliofurika Uwanja wa Amaan, kisha akapokea salamu za heshima kutoka kwa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa na vikosi hivyo, huku mizinga 21 ikipigwa kwa heshima ya Rais.
Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi wakuu wa kitaifa kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi, pamoja na Marais Wastaafu wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein na Dkt. Amani Abeid Karume.
Viongozi wengine waliokuwepo ni Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wawakilishi wa vyama vya siasa, Mabalozi wa nchi mbalimbali, na wawakilishi wa Jumuiya mbalimbali za Kimataifa walihudhuria sherehe hizo za kihistoria.
Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi anaanza rasmi kipindi cha pili cha miaka mitano (2025–2030) cha kuiongoza Zanzibar, akiendelea na dhamira yake ya kuimarisha amani, umoja, uwajibikaji, na maendeleo endelevu kwa wananchi wa Zanzibar.





Maoni yako